Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, February 4, 2014

ZIARA YA RC KANDORO SIKU YA KWANZA MBEYA VIJIJINI

Ziara ya mkuu wa mkoa wa Mbeya Abass Kandoro(Mwenye suti ya kaki) ilianzia katika Mradi wa ujenzi wa banio la maji kwaajili ya kuwezesha kilimo cha umwagiliaji katika kijiji cha Imezu unaoendelea.Akiwa hapa Kandoro akaelezwa namna kikundi cha wajanja wachache kilivyotaka kutafuna fedha kiasi cha shilingi milioni 208 kilipoomba kutoka halmashauri ya wilaya ya Mbeya kwa madai kuwa kilitaka kujenga mradi wa kilimo cha umwagiliaji.Baadaye ilibainika kuwa wanakikundi hawakuwa wakazi wa kijiji hicho na ndipo halmashauri ikachukua uamuzi wa kusitisha matumizi ya fedha hizo ambazo zilikuwa zimekwisha inginzwqa katika akaunti ya kikundi hicho. Hata hivyo hadi mkurugenzi wa halmashauri anasitisha matumizi ya fedha hizo tayari wajanja hao walikuwa wamekwishachota kiasi cha shilingi milioni 21.Baadaye kiasi kilichosalia halmashauri ilichukua maamuzi ya kuwasaidia wakazi halali wa kijiji cha Imezu kujenga banio hili hivyo ilihamisha fedha kutoka akaunti ya kikundi cha wajanja wajanja na kuingiza katika akaunti ya kijiji kiasi cha shilingi 187,139,000 ambazo ndiyo zinatumika kutekeleza mradi huu.Agizo la Kandoro ni kuwa ifikapo kesho asubuhi(Februari 5) kaimu mkurugenzi awasilishe taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliotafuna milioni 21 ikiwa ni pamoja na maafisa kilimo waliohusika kupeleka fedha hizo kwenye akaunti ya kikundi cha wezi kwani fedha hizo lazima zirejeshwe.Kandoro pia ameagiza asubuhi hiyo hiyo kaimu mkurugenzi amfikeshe ofisini kwake afisa aliyetelekeza mizinga iliyokabidhiwa wakati wa mbio za mwenge kwa vikundi vya wafugaji lakini haijawekwa mahali husika hadi mkuu huyo wa mkoa alipoikuta imetelekezwa pembezoni mwa bara bara wakati akitoka kijiji cha Itewe kwenda kijiji cha Wambishi kata ya Ulenje. Akiwa katika kijiji cha Itewe aliweza kutembelea shamba la mmoja wa wakulima walionufaika na mpango wa serikali wa kutoa pembejeo ya mbolea kwa wakulima wasio na uwezo.Haya ni sehemu ya mafanikio ya mpango huo. Ziara ikaendelea hadi katika shule ya sekondari ya Itala iliyopo katika kata ya Ulenje.Hapa ni kutembelea mradi wa maabara ya shule hii ya kata. Hapa mkuu wa mkoa akimsikiliza mkuu wa shule hiyo alipokuwa akizungumza changamoto ikiwemo wazazi kutokuwa na hamasa ya kuchangia chakula kwaajili ya watoto ili wapate chakula shuleni hapo. Ziara kwa siku hii ya kwanza ikamalizika kwa kutembelea jengo la machinjio mapya yanayotarajiwa kuwa ya kisasa.Machinjio haya yanajengwa katika kata ya Utengule Usongwe.Mkuu wa mkoa ameitaka halmashauri kutafuta mbinu mbadala itakayowezesha kupatikana kwa fedha kwaajili ya kukamilisha ujenzi huo.Moja ya njia sahihi alizoshauri ni kutafuta mwekezaji atakayekubali kuingia ubia na halmashauri kukamilisha ujenzi huo na machinjio yatakapokamilika kutokana na mkataba wa kimakini utakaokuwa umewekwa awe mwekezaji na kuanza kukata kiasi alichowekeza kwenye kodi anayopaswa kuilipa halmashauri.

No comments:

Post a Comment